Shule ya Sekondari Santakagwa.

SERA YA ELIMU (RASIMU)

SERA YA ELIMU (RASIMU) SANTAKAGWA SEKONDARI


UTANGULIZI

Elimu ni mwongozo unaomwezesha mtu kupata maarifa na mbinu muhimu za kuyakabili na kuyakubali mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa na kiuchumi na kutumika kama nyenzo ya mtu kutambua na kutumia vipawa vyake. Hapa kwetu Tanzania elimu inasisitiza uzalendo, ustadi na kudumisha tunu bora katika tamaduni na desturi zetu. Kwa njia ya elimu mtu hushirikisha mang’amuzi yake, uvumbuzi mpya na tunu zote katika historia ya maisha yake katika kuishi a kujiendeleza na hivyo huifanya na kuisaidia jamii yake hususani hii jamii yetu ya Santakagwa.


SERA HII YA ELIMU YA SANTAKAGWA SEKONDARI

Sera hii ya elimu ya Santakagwa Sekondari imeandaliwa ikizingatia miongozo mbalimbali ya wizara ya Elimu Sayansi Teknolojia na mafunzo ya ufundi kwa sera yake ya mwaka 1995 na rekebesho lake ni mwaka 2002 pasipo kukosa kufumbata tafiti madhubuti zilizofanywa na mmiliki kwa kuamini kuwa Elimu kwa maana ya ufahamu, ujuzi, maarifa, kusaidia na kumkomboa binadamu na kuweza kumtumainisha kimaisha kwa nyanja ya kisiasa, kiuchumi, kijamii mintarafu kifikra kuweza kukomboleka.

Shule yetu ya sekondari Santakagwa inajitahidi kutekeleza haya yaliyoelezwa katika sera kwa vitendo ili kutimiza lengo lake kuu la kumkomboa binadamu kimwili hususai kiuchumi na kiroho pale itakapobidi.


1. MAANA YA SERA

Kidhana sera ni mwongozo na utaratibu wa kufikia malengo maalum. Santakagwa sekondari imekuwa ikijishughulisha na utoaji wa elimu takribani kuanzia mwaka 2010 japo imeibuka vilivyo pale iliposajiliwa rasmi mnamo 21/01/2013. Aidha Santakagwa inatambua kuwa utoaji wa elimu ni huduma muhimu katika kazi ya uwekezaji katika raslimali za msingi, elimu inamsaidia binadamu kuongeza ufanisi wake wa kazi na hivyo kuweza kuzalisha zaidi au kutoa huduma bora zaidi. Bila kazi hii haiwezekani kuyaendeleza maisha ya binadamu, elimu humsaidia binadamu kutoka katika hali duni na kwenda katika hali bora ya maisha.

1.1 Sera ya elimu Santakagwa ni mwongozo wa kuandaa Taifa la Tanzania na hususani jamii ya wanarukwa kuweza kupata elimu na maadili kwa manufaa ya watu wote. Hivyo basi sera hii itajulikana kama SERA YA ELIMU SANTAKAGWA SEKONDARI – SUMBAWANGA. Hii ndiyo sera itakayo tumika kama dira (mwongozo) ya utekelezaji wa mambo yote ya elimu yanayo simamiwa na Mkurugenzi (mmiliki). Sera hii itakuwa mkataba kwa yeyote atakaye kuwa ameajiriwa au anasoma katika shule hii na hivyo itakuwa na nguvu ya kisheria mwenye kukiuka hatua za kinidhamu zitachukuliwa kulingana na uzito wa ukiukaji ikiwa ni pamoja na fidia kwa dhara lolote litakalosababishwa na ukiukwaji huo.


1:1:1. DIRA (VISSION)

Kuwa na mtu au mwanajamii aliye elimika kwa kiwango cha juu mwenye maadili stahiki, stadi na mwelekeo mwema kimwenendo kwa ukadili wa mila na desturi za jamii yetu. Zaidi awe mahili na aliye tayari kukabiliana, kushiriki kwa ufanisi katika kuyafikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na taasisi yetu na taifa kwa ujumla.


1:1:2. DHIMA (MISSION)

Kuwezesha/kutoa elimu bora na maadili mema kwa watu kwa kushirikiana na wadau wengine.


1:1:3 TUNU/THAMANI (VALUES)

Kuthamini na kuzingatia mila na desturi za kitanzania na Afrika kwa ujumla hususani mfanowe wanarukwa.


1:1:4 MALENGO AU SHABAHA YA ELIMU (Aims /goals)

Shabaha ya elimu ni kuleta mabadiliko chanya yatakayo msaidia binadamu aweze kuishi vizuri kwa kujiletea maendeleo ya kweli yenye kutunza utu na thamani ya binadamu.


LENGO MAHUSUSI

Ili kuweza kufikia azima ya kutoa elimu, Santakagwa imejiwekea malengo yatakayowezesha kupima hatua ili kufikia na kutekeleza malengo yake hivyo ili kutekeleza dhima iliyojiwekea na ndoto (dira) yake inayofikiriwa (strategic plan):-

  1. Kutangaza ukombozi kwa watu wote kwayo watu wote watajikomboa kinyanja.
  2. Kuchangia katika utoaji wa elimu na upatikanaji wake nchini hivyo taifa litafaidika kutokana na taasisi kutoa nafasi ya elimu.
  3. Kuimarisha uwezo wa mtu na jamii katika kutatua mitazamo mibovu na badala yake kuimarisha desturi zilizo njema.
  4. Kutekeleza sera ya taifa ya elimu na mafunzo ya ufundi (1995) ya kumwezesha mzawa/mtu awaye yote kujitegemea ( education for self reliance) kwa kusema uzingativu wa dira ya taifa na mikakati ya maendeleo ndio chimbuko la maendeleo hivyo wananchi ndio chimbuko na walengwa wakuu na wadau katika utekelezaji wa sera.
  5. Hivyo ni vema elimu ikazie kujifunza kwa vitendo kwamba shughuli zote za uzalishaji na miradi zitahimizwa katika shule na vyuo vyetu. Wanafunzi wahusishwe katika miradi ya shule kama vile kilimo, ufugaji wa wanyama wa aina zote, duka la shule, bwawa la samaki na nyinginezo. Ni jukumu la bodi na kamati za shule kuona shule zetu zina miradi ya aina mbalimbali yenye kuongezea pato la shule yetu.
  6. Kuwalea vijana katika maadili mema ya kijamii..

HISTORIA YA SHULE YA SEKONDARI SANTAKAGWA KWA UFUPI

Shule hii ya Sekondari Santakagwa inamilikiwa na mwalimu Linus Mizengo, ilianza rasmi mnamo tarehe 09/01/2010 imesajiliwa mwaka 2013 kwa namba S.4667 na namba ya kituo cha mtihani S.5053 na P.5053.

Ni shule ambayo imekuwa ikinukia mapito chanya kwa nyanja ya kitaaluma na kimaadili; hatuna historia ya kupata daraja la nne (division four) na sifuri; kwa uchache sana tena kwa nadra tunapata daraja la tatu (division three). Daima matokeo yetu yamekuwa yaking’ara kwa ufauru wa daraja la kwanza na la pili (division one &two). Hii ni kwa kidato cha pili na cha nne.

Tunafundisha kwa kuuisha (mentoring) ili mwanafunzi ajitambue na elimu imsaidie kimaisha. Pia tunahakikisha kuwa shule yetu inaimarishwa vema kwa misingi bora ya kitaaluma na kimaadili kwa wanafunzi wetu kwa kuzingatia mitaala mipya ya wizara ya Elimu napia kuzingatia utumizi sahihi wa lugha ya kufundishia ambayo ni Kiingereza.

Zaidi mfumo wa ratiba yetu kuu ya kila siku inampa mwanafunzi fursa ya kuweza kujifunza vema masomo yakini na ya kimalezi (somo la maadili). Sambamba na hilo tunao walimu wakutosha waliobobea kitaaluma katika ufundishaji wa kuzingatia mitaala ya wizara ya elimu, zaidi tunayaona matunda ya ufaulu wa mitihani ya ndani na nje, changamani, Mock na ya taifa tunaonekana kufanya vema. Kama ilivyo elezwa hapo awali yakuwa ni matokeo chanya ya bidii ya walimu na watumishi wasio walimu kwa malezi fungamano, Lugha ya mawasiliano hapa shuleni ni Kiingereza tu katika nyanja zote na miundombinu ya shule ni salama na bora kwa mtoto/mwanafunzi kupata elimu iliyo bora.

Ni dhahili tunatoa elimu yenye kumwezesha mtoto wa kitanzania kuweza kujimudu katika maisha ya kila siku kwa kadili ya mazingira na mstakabali wa maisha yake. Hivyo rai kwa mzazi/mlezi fanya chaguo lako liwe Santakagwa Sekondari katika maamuzi ya kumpatia mwanao elimu bora yenye tija.